Tuesday, November 13, 2007

Chalenji haina maana kwa akina McCarthy wetu

Chalenji haina maana kwa akina McCarthy wa kwetu


Na edo kumwembe NI michuano mikubwa na ya kihistoria katika ukanda huu, lakini ni wakati wa kuchunguza kama michuano hii ya Chalenji ina manufaa kwa soka letu. Si kama michuano hii haikuundwa kwa mfumo wa kulisaidia soka la Afrika Mashariki na Kati, hapana tatizo kubwa ni tofauti kubwa ya kiuchezaji na kimadhumuni iliyojitokeza katika miaka ya karibuni miongoni mwa wachezaji wa ukanda huu. Kwa mfano, inaonekana wazi nchi za Uganda na Kenya zimekuwa zikiitumia michuano hiyo kwa ajili ya kukuza wachezaji wake tegemeo wa siku za usoni na si kuchezesha nyota wake kwa ajili ya kunyakua tu taji hilo. Kwa mfano, Uganda ina wachezaji wake mahiri ambao nina uhakika hawawezi kugusa michuano ya Chalenji hata kama wangeweza kuruhusiwa na vilabu vyao. Wachezaji wengi watakaokuja ni wale makinda ambao walikuja kucheza na Stars katika mechi ya kirafiki Septemba mwaka huu. Itakuwa vigumu kuwaona nyota wanaocheza Ulaya kama Charles Livingstone Mbabazi anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya St Patrick ya Ireland akija nchini kwa ajili ya kucheza michuano ya Chalenji. Sitegemei kumuona David Obua wa Kaizer Chiefs na kipa Dennis Onyango wa Supersport United wakiwasili nchini kucheza michuano hiyo. Kwao hii ni michuano ya kutafuta kina Onyango wengine na hapana shaka wanafanikiwa kwa mtindo huu. Hadithi hiyo inakwenda kwa Wakenya. Katika michuano kama hii hawawezi kuwaita kina Robert Mambo, Dennis Oliech wala McDonald Mariga wa Parma ya Italia. Hawawezi pia kumuita Mussa Otieno anayecheza Afrika Kusini. Kifupi wenzetu wanaigeuza michuano hii kama vile ambavyo wenzetu wa nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika walivyoigeuza michuano ya COSAFA katika kusaka vipaji vipya. Kule huwezi kuziona sura za akina Collins Mbesuma, Ben McCarthy, Aaron Mokoena, Nasief Morris, Macbeth Sibaya, Sibusiso Zuma, Steve Pienaar, Benedict vilakazi na wengineo wakichezea Afrika Kusini na Zambia katika michuano ya COSAFA. Lakini kwetu michuano ya Chalenji ni fainali kubwa sana. Sielewi ni kwa nini hali hii inatokea kwa wenzetu lakini kwetu ni tofauti. Inawezekana ni kwa sababu hatuna nyota wengi wa kulipwa nje ya nchi na ndio maana tunaigeuza michuano hii kama ëdilií kubwa katika kuwaona nyota wetu. Nakumbuka mwaka jana wakati michuano hii ilipofanyika Ethiopia, kocha Marcio Maximo alijaribu kutumia falsafa ya wenzetu katika kuhakikisha nyota chipukizi wanakwenda na wale wakongwe kina Nsajigwa Shadrack, Victor Costa, Ivo Mapunda na wengineo wanabakia nyumbani. Mashabiki walichachamaa sana bila ya kuelewa falsafa hii rahisi lakini nadhani sasa ni wakati wa kubadili mtazamo na kuangalia ni namna gani tunaweza kuitumia michuano hii. Nafahamu itakapoanza mashabiki na viongozi wa soka watataka mambo makubwa sana kutoka kwa wachezaji na jopo la ufundi, bila kujua namna tunavyoweza kuyatumia mashindano haya katika kukuza zaidi vipaji kuliko kuwatumia sana kina Nsajigwa ambao wameshathibitisha kile wanachoweza kukifanya katika ngazi za kimataifa. Binafsi sijaona hata umuhimu wa kuwaita Danny Mrwanda na Nizar Khafani katika michuano kama hii. Kama wanapata uzoefu wa kweli katika soka la kulipwa ni kiasi cha kuwanyanyua wachezaji wengine tu ili waweze kufikia kiwango chao. Sidhani kama itakuwa vigumu kwa kocha Maximo kuwaunganisha nyota hawa wa kulipwa na wengineo waliopo nyumbani kwa sababu inaaminika nyota wa kulipwa wanafundishwa na walimu wa kisasa wa kiwango cha Maximo huku uwezo wao wa kuelewa ukiwa juu zaidi. Kama mna timu ambayo kwa kiasi chake imeanza kujaribu kucheza na Senegal, Burkina Fasso na Msumbiji, nadhani mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya timu hizi zinaweza kuwa muhimu zaidi kuliko michuano ya Chalenji. Wachezaji wetu wametuangusha kwa kiasi kikubwa. Kama kina Haruna Moshi wangekwenda kucheza soka la kulipwa nadhani ilikuwa nafasi kwetu kuwaona nyota waliochipukia katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea. Lakini kwa akina Haruna kucheza na wachezaji wapya waliochaguliwa na Maximo ni kuyumbisha maana nzima ya michuano ya Chalenji ambayo kwetu tunapaswa kuitumia katika kuanzisha kizazi kingine cha soka kama wenzetu. Kwa barani Ulaya unaweza kuipima michuano hii na ile ya Olimpiki. Timu zinachagua nyota chipukizi na kuongeza nguvu kwa kuchukua nyota watatu wazoefu kwa ajili ya kunogesha timu. Nafikiri kuna tatizo moja litamsumbua sana Maximo. Tatizo la kujua namna ya kukabili michuano inayomkabili pamoja na kukuza soka letu kwa ujumla. Kama kocha amechagua kikosi hiki kwa madai ya kujiandaa na mechi za kufuzu kwenda Kombe la Dunia 2010 pamoja na kuibua vipaji, nadhani kuna kimoja kinaweza kufaulu na kingine kikafeli vibaya. Ni namna gani mashabiki wanaweza kumuelewa, nadhani huo ni mtihani mkubwa kwake kutegemea tu na aina ya mashabiki wetu tulionao nchini. Mwisho wa yote nafikiri itanifurahisha kuona wachezaji wengi waliochaguliwa kwa mara ya kwanza kutoka timu za mikoani wakicheza katika michuano ya Chalenji na kisha wakiibuka kwa kujiamini zaidi, kuliko kuwatumia kina Haruna na kushinda huku tukijifurahisha tu katika nafsi zetu bila ya kusonga mbele. Ni wakati wa kuifikiria upya michuano hii. Wenzetu wanaitumia kwa akili zaidi pengine kuliko sisi ambao unazi umetujaa tukitamani kushinda kila kitu bila ya kujua kama tunasonga mbele au tunarudi nyuma. Naomba kutoa hoja waheshimiwa.

3 comments:

kelvin fella said...

Nimesoma makala yako yenye kichwa cha habari chalenji haina maana kwa akina McCarthy wetu. Ni makala nzuri inayoonyesha jinsi gani soka la nchi hii hailiwezi kuinuka kwa kutegemea michuano ya chalenji. Ukiangalia wanachama wa CECAFA ambao ndio waandaaji wa michuano hii ya chalenji utaona jinsi gani walivyo wachovu watupu, Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Somalia, Eritrea, Djibouti, Zanzibar hakuna nchi yenye historia ya kuvutia katika soka isipokuwa tu Sudan na Ethiopia ambao walikuwa wanafanya vizuri katika miaka hile ya 1960s na 1970s lakini kwa sasa choka mbaya, mfano mzuri ni nchi zinazofuzu kushiriki kombe la Afrika ukanda huu umekuwa nyuma miaka yote na hii si kwa bahati mbaya kama ambavyo baadhi ya wadau wamekuwa wakisema, mwaka huu tumeingiza Sudan pekee kwenye CAF 2012, kufuzu kombe la dunia zimekuwa ndoto za miaka mingi na hizo ndoto zitaendelea kuwepo kwa kadiri ninavyoona uelekeo wa soka la ukanda huu limekuwa linazidi kupwaya. Kwa kiwango hiki cha soka tulichonacho katika ukanda huu wa Africa mashariki ni bora michuano ingebaki kuwa ya wachezaji wanaocheza soka la ndani kama ilivyo CHAN ili kuinua viwango vyao au ibaki kuwa michuano ya vijana aidha chini ya miaka 23 kama olimpiki au chini ya miaka 17 au 21. Katika miaka michache iliyopita CECAFA iliwahi kuanzisha michuano ya vijana chini ya miaka 21 na 17 sijui ilikofia michuano hii kwani niliiona kama mkombozi wa soka letu la vibonde wa Afrika kwani ingekuwa rahisi kuibua vipaji vingi vipya na kuvutia mawakala kuliko ambavyo yanakuwa mashindano ya wanaume wa zaidi ya miaka 30. Mwaka jana wabongo tulibeba kombe la chalenji lakini hicho tu si kielelezo cha kupanda kwa soka letu au ubora wa timu yetu kwani tulikuwa washindi kwa vibonde kama tumeshindwa kufuzu CAF, wapo wanaosema mbona Nigeria, Cameroun, Misri na Afrika kusini wameshindwa kufuzu lakini wanasahau rekodi ya nchi hizi na mafanikio waliyo nayo kisoka kwangu mimi kushindwa kufuzu kwa nchi hizi naweza kusema vitu viwili tu kwanza ni kuteleza lakini pia ni kupanda viwango kwa baadhi ya nchi hili si geni limewahi kuzitokea nchi nyingi tu mfano England ilishindwa kufuzu Euro 2008 kwa bahati mbaya kwani walikuwa na timu nzuri tu yenye watu kama Beckham, Gerrald, Lampard, Terry, Ashley Cole, Rooney na wengineo lakini pia tusisahau na kiwango cha wababe wao (Croatia) katika michuano hiyo kilikuwa juu sana. Kwa hapa Afrika, Nigeria, Cameroun, Afrika kusini walishiriki kombe la dunia 1998, 2002 wakashindwa kufuzu 2006 wakarudi 2010 naamini tutaendelea kuwaona katika michuano ijayo, si kama sisi tunaolilia bahati wakati viwango vibovu. Wana East Africa tujipange bado tuko m

Anonymous said...

Mimi ni ndugu yako natokea kijiji cha Mbessa TUNDURU ni mwl hapa Dar nakumbuka nilikuona pale Habari House bnamagono@gmail.com 0717347312

Anonymous said...

Imani kadhaa,hazihafiani na neno kurogwa,ninapenda kutumia neno hili na hakika watanzania wengi wanelewa.Viongozi wetu kwa ngazi zote,nadriki kusema kwamba,WAMEROGWA.Hapa nakubaliana na hoja yako.TFF inaendeshwa na watu ambao itikadi zao na sala zao ni USIMBA na UYANGA na FEDHA.Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.Rais wetu alionesha njia kuelekea soka la kweli,lakini nadhani naye pia ana mapenzi makubwa upande mmojawapo,hivyo ule usimba na uyanga umefanya kazi yake hadi ikulu.Lakini awamu ya nne ndo inakamilishwa 2015 tukiwa mbali na ndoto za kufuzu fainali za mataifa ya Afrika na dunia.Na labda hapa kwetu tatizo letu ni mfumo,kwani ni nchi inayoendeshwa na MAKOMUNISTI.Itikadi hii hufanya mali ya umma kuwa ni mali ya kuendesha mfumo uliopo yaani kwa masilahi ya familia zao.Sheria ya historia inasema ni kuondoa mazoea yaliyopo,na hii huamuliwa kwa kuweka sheria au kwa ufupi ni kubadili katiba iliyopo ili kufanya utendaji zaidi kuliko ilivyo sasa.kijanitz.blogspoprt.com