Tuesday, November 13, 2007

nani anaijali hatima ya Tanzania?


Nani anaijali hatima ya Tanzania?

Na edo kumwembe

Ni nchi ya ajabu kwa mwanadamu makini kuweza kuishi. Ni nchi inayoshangaza sana, ingawa raia wake hawaonyeshi kushangazwa na matukio kadhaa yanayotokea.

Naizungumzia Tanzania nchi niliyoishi kwa miongo kadhaa tangu nizaliwe. Baada ya nyimbo nyingi za matatizo, dhiki, wizi, rushwa, tabu, magonjwa na kila aina ya shida ambayo mwanadamu wa kawaida anapitia, jawabu kubwa linapatika kwa swali; nani anajali?Ndio, nani anajali? Hili ni swali ambalo kila Mtanzania anapaswa kuulizwa.

Ni kwa kiasi gani, mwananchi wa kawaida, kiongozi au muhusika yeyote wa nchi hii anajali matatizo ya nchi yetu.Nimejaribu kwa kiasi kikubwa kutazama sura za viongozi wetu, mawaziri, wabunge, Wakurugenzi, Mameneja na kila kiongozi. Sioni anayejali.Wengi wanaongea wasichofikiria kukifanya kwa dhati na nchi imezidi kuoza. Akili zao ziko katika wizi kwa sababu na wananchi wenyewe wala viongozi wengine hawajali.Nchi inatafunwa kila jua linapochomoza na kuzama. Hakuna anayejali na kila mtu anaangalia maisha yake.

Msukuma mkokoteni haoni ni kwa namna gani anahusika na Waziri mwizi wala Mkurugenzi wa Manispaa mla rushwa.Atajihusisha vipi? Kwa nini atumie muda wake mwingi kujali? Kama watu wanaomzunguka hawajali kula yake kwa nini na yeye awe anajali maisha ya wengine.Siwezi kusema nilifaidi matunda ya utawala wa Mwalimu Nyerere. Sijui mengi yaliyotokea wakati wa Utawala wake, lakini tangu nilipopata akili timamu sijawahi kusikia Rais wa nchi yangu akimfukuza kazi Waziri wake kwa rushwa wala wizi.

Je ni kweli kwamba marais wangu hawawaoni Mawaziri wezi na wala rushwa? Kama wangekuwa watiifu na waadilifu basi nchi yetu ingekuwa mbali. Lakini naamini wanawaona, kikubwa ni kwa vile hawajali kinachotokea.

Hawajali kwa sababu hawana sababu ya kujali. Kwa kuwa wananchi hawajali basi na wao hawajali kama ambavyo wananchi hawajali. Wanaendelea kutojali na daima tunaendelea kupata vizazi vya Watanzania wasiojali.Kwani tukifungua mikataba ya ajabu ya Madini hatuwaoni walioweka saini hizo? Tunawaona, lakini nani anajali? Nchi inasonga mbele na maisha yanaendelea.

Huyu anajaribu kuandika gazetini kwa uchungu na yule anatamka lile katika kipindi cha redio kwa uchungu, lakini nani anajali? Kina mama na watoto wanafungulia michezo ya maigizo ITV na kwingineko. Nani atawalaumu wakati watu makini wenyewe hawajali? Si afadhali nao wasijali!Kwani yuko wapi yule Waziri aliyesema yuko tayari kuona wananchi wanakula majani ili ndege ya Rais inunuliwe? Ndege ambayo ni mbovu!. Si amechaguliwa tena kuwa Waziri? Nani anajali kama Rais wa sasa hakujali? Mimi nitajali nini?

Ni mwananchi gani anajali? Walio wengi wanafanya maaandamano katika mikasa ya kidini au ile ya kumpongeza Rais aliyefutiwa madeni ambayo fedha zake zilitumiwa kununua mashangingi.Kuna anayejali kwenda katika maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya umeme? Kuna anayejali kuandamana baada ya kusikia Nesi amesababisha kichanga kufa sekunde chache baada ya mama mjamzito kujifungua?

Hakuna anayejali kwa sababu hata akiandamana kwa uchungu mkubwa, Rais hawezi kumwajibisha Waziri wa Afya!. Ndivyo nchi ilivyo na watu wengi wamekwenda jela baada ya kutoa taarifa njema kwa jeshi la Polisi.

Lakini nani anajali kuwepo kwao jela? Ukitoa taarifa kuhusiana na mkubwa fulani anayepokea rushwa, kesho yake Kamanda wa Polisi wa Mkoa anakuonya na kukwambia uachane naye.Kwa nini niendelee kujali kwa watu ambao hawajali? Watu wangapi walishikwa na madawa ya kulevya katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam lakini wapo nje kwa madai kwamba uchunguzi unaendelea?

Uchunguzi upi wakati madawa yalitolewa tumboni na tukaonyeshwa katika taarifa za habari za Televisheni mbalimbali? Kwa nini niendelee kujali kuwepo nje kwa mtuhumiwa wakati Kamanda wa Polisi wa mkoa haonyeshi kujali?Yuko wapi dada machachari Mbunge wa kike aliyedai kwamba ana majina ya wauza madawa wa kulevya? Ni kweli kwamba alizungumza jambo jipya katika jamii yetu ya watu wasiojali?

Tunao watu wengi wanaouza madawa na kwa bahati wanajulikana, lakini nani anajali? Dada yule ‘alionyesha’ kujali, lakini baada ya hapo nani amejali? Mbona hatujasikia mtu amekwenda ndani kutokana na mdomo wake?Tangu baada ya ‘mauaji’ ya basi ya Buffalo, magari yanazidi kwenda kasi barabarani. Nani anajali? Si mpaka watu wengine wafe ndio tusikie tamko jingine la kinafiki?Kuna meli ngapi mbovu pale Ziwa Victoria na sehemu nyingine zenye vyombo vya usafiri wa majini? Kwa sababu hakuna anayekufa kwa sasa wahusika na wananchi hawajali mpaka litokee janga.

Ili mradi asubuhi inafika, mchana unapita na jioni inawadia basi hakuna anayejali mpaka litokee janga. Nani anajali?Mchele mbovu unahalalishwa, watu wanatengeza maji ya ‘kufoji’ na kuuza, nani anajali? Nikienda kusema Polisi wananitazama kwa jicho la chuki lakini tayari nimeshawaachia mianya ya rushwa.

Keshokutwa nakutana na mkubwa wa Polisi niliyemshtua akiwa pamoja na mkuu wa Kiwanda nilichokishtaki. Wanakula ‘kitimoto’ pamoja na wanacheka vilivyo, nani anajali?Kuna watu wachache walikiweka mikononi Chama cha soka nchini FAT,enzi hizo. Nani alijali? Kama si kuvurugana wenyewe kwa wenyewe wangeweza kuwepo mpaka leo.Ndio, Rais wa nchi alikuwepo, lakini hakuwa na muda wa kujali. Kipaza sauti kilikuwa kinamwambia asijali mambo hayo ila aelekeze macho katika Utandawazi.

Ndio, utandawazi ambao unaruhusu tupeleke makontena ya mchanga uliochanganyika na dhahabu nje ya mipaka yetu. Nani anajali?Wachache wanajaribu kujali lakini nani anawasikia? Wenyewe wanakutana Golden Tulip wakila firigisi na kupeana ruhusa hizo. Mimi na wewe tujali nini wakati hatuna uhakika wa kesho?

Tukipata watoto nao wanaingia katika mkumbo huo huo wa kutojali. Kizazi hiki ambacho watoto wengi wamegeukia hisia za kimagharibi ni yupi kati yao anaweza kujali?Wa kiume anakazania kusuka, wa kike anatamani kuvaa kama Beyonce. Hakuna hata mmoja mwenye hisia na nchi. Hawezi kujali kwa sababu hajafundishwa kujali.

Ukisikiliza maoni ya wengi kuhusiana na kesi ya Justine Kasusura, wengi wanamlaumu kwa nini hakutoweka nje ya nchi. Hakuna anayesikitika kwa kitendo chake cha kuiba fedha. Kwa nini?Watu hawajali alichokifanya. Yeye alifanya hadharani lakini kuna wanaoiba kwa karatasi? Hawa akina ‘Kasusura’ wa mezani nani anawazuia? Nani anawajali?Iko wapi Kampuni ya Richmond? Mbona kimya? Nani anajali? Kwa sasa umeme upo na watu hawajali tena. Wanataka ije ‘Richmond’ nyingine ya Maji au huduma za Afya. Nani anajali?

Ndio, sijawahi na wala sitaki kupiga kura. Yupo atakayesema napoteza haki yangu ya msingi. Simuoni wa kunijali na hata kama akiamua kunijali basi mfumo hauwezi kumsapoti anijali.Wakati wananchi wengine wakipiga kura mimi naangalia vipindi vya soka katika Televisheni, kwa nini uniambie sijali wakati atakayechaguliwa hatanijali?

Katika kituo cha wapiga kura chenye wakazi 1000 lakini mshindi ameshinda kwa kura 1200, kwa nini nijali kusumbuka juani huku FFU wakinighasi wakati waliopanga matokeo hawaijali kura yangu?Nijali nini hasa kwa kutompigia kura mtu atakayekwenda bungeni kupitisha sheria ya Takrima? Acha nifuatilie Ligi kuu ya England na utamu wake.

Soma magazeti yetu ya leo. Watu wameamua kuandika mambo laini ambayo si sehemu ya mapambano yetu.Makala za leo ni zile zile zinazoelezea kwa undani Habari za Theolojia, Ulokole, na mambo mengine. Mwananchi asiye na uhakika na machweo ataelewa nini na kupata tumaini jema katika makala hizi? Wanaoziandika hawajali kinachotokea kwa sasa.

Kwetu, kiongozi kutajwa anamiliki hiki na kile kwa jina la mwanae, si kashfa. Kwetu, mtoto wa mkubwa au mkubwa mwenyewe kuua si jambo la ajabu sana. Nani anajali? Wao na Kamanda wa Polisi wanakutana Kilimanjaro Kempsky katika dhifa mbalimbali, unajua wanaongea nini? Kwa nini ujitie kimbelembele cha kujali? Ili mradi unapumua, iangalie siku yako ya kesho.Tanzania ya leo imejaa watu wanaozijali familia zao.

Nani atawalaumu watu hawa? Kwani viongozi wetu wanawajali kina nani? Si wanajali elimu za watoto wao pale Oxford, Havard na kwingineko?Kama unabisha, mbona sasa hivi ndio wanatuongoza? Nani anajali? Tuna uhakika gani kama baadaye wajukuu hawataongoza? Si ndio wanapewa ukamanda wa vijana wakijiandaa kumtawala mwanangu ambaye ni mnyonge wa baadaye? Nani anajali?Sina hasira na mtu.

Nina furaha na maisha yangu kwa sababu napata ninachokitaka kwa uhalali. Kama maisha yataendelea kuwa hivi basi nisilaumiwe kwa kutojali. Nina uhakika gani kama wenzangu wanajali?Kilio kama changu kimetamkwa mara ngapi na watu makini? Nani amejali? Kelele za mchanga wa dhahabu nani amezijali?Waliongia mikabata mibovu ya madini nani anawajali? Wangekuwa Chini,Japan, Uingereza na kwingineko, wangekuwa wapi watu hawa kama si katika kuta za Gereza? Hapa kwetu nani anajali?Lakini nijali nini zaidi wakati Rais wa nchi aliwahi kuwatamkia watu walioelezea hisia zao kwa Waziri Mkuu wake kuhusu umilione wake wa mashaka, kwamba wana wivu? Kama yeye mtu wa juu kabisa hakujali, nani atajali?Utawala ule ulikumbana na migomo ya wanafunzi, huu nao unakumbana na migomo hiyo hiyo, nani anajali? Kuna njia za kudumu za kumaliza migomo hiyo ambayo nimeisikia tangu utotoni mwangu?Huyu anakabiliana nayo leo, akihamishiwa anahama na hisia zake. Yule anakuja na hisia nyingine na wala hajali kutazama alipoishia mwenzake.

Leo, kuna watu wengi wanapiga kelele kuhusiana na hatari ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nani anawasikiliza? Mimi naweza kuwa sehemu ya maamuzi hayo?Wanaotoa tahadhari ni watu wasomi. Afadhali ingekuwa kwangu mtu nisiye na elimu, lakini wanaotoa tahadhari hizi ni watu wanaoheshimika kwa elimu na upeo wao.

Najua hawasikilizwi lakini nani anajali? Kama wenzao hawajali, nani atanisikiliza mimi nisiye na lolote? Acha waamue nami nitatii kwani waliamua mangapi ya hatari na nimeendelea kutii? SijaliLakini kwa nini nimewang’angania wasiojali wakati hata wenyewe wakifa au kuondoka madarakani hakuna anayewajali?

Wako wapi waliojali ambao familia zao zinaishi kama vile baba zao hawakujali? Ndio, familia za akina Edward Sokoine. Nina uhakika watoto wao watajuta kwa kitendo cha baba yao kujali sana wakati wa utawala wake.Ndio, na hata ninapomaliza kuandika makala hii, wengi wataelewa ninachomaanisha. Wakubwa wengi na watu wa kawaida wataisoma na kuielewa. Lakini nani atajali?

Chalenji haina maana kwa akina McCarthy wetu

Chalenji haina maana kwa akina McCarthy wa kwetu


Na edo kumwembe NI michuano mikubwa na ya kihistoria katika ukanda huu, lakini ni wakati wa kuchunguza kama michuano hii ya Chalenji ina manufaa kwa soka letu. Si kama michuano hii haikuundwa kwa mfumo wa kulisaidia soka la Afrika Mashariki na Kati, hapana tatizo kubwa ni tofauti kubwa ya kiuchezaji na kimadhumuni iliyojitokeza katika miaka ya karibuni miongoni mwa wachezaji wa ukanda huu. Kwa mfano, inaonekana wazi nchi za Uganda na Kenya zimekuwa zikiitumia michuano hiyo kwa ajili ya kukuza wachezaji wake tegemeo wa siku za usoni na si kuchezesha nyota wake kwa ajili ya kunyakua tu taji hilo. Kwa mfano, Uganda ina wachezaji wake mahiri ambao nina uhakika hawawezi kugusa michuano ya Chalenji hata kama wangeweza kuruhusiwa na vilabu vyao. Wachezaji wengi watakaokuja ni wale makinda ambao walikuja kucheza na Stars katika mechi ya kirafiki Septemba mwaka huu. Itakuwa vigumu kuwaona nyota wanaocheza Ulaya kama Charles Livingstone Mbabazi anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya St Patrick ya Ireland akija nchini kwa ajili ya kucheza michuano ya Chalenji. Sitegemei kumuona David Obua wa Kaizer Chiefs na kipa Dennis Onyango wa Supersport United wakiwasili nchini kucheza michuano hiyo. Kwao hii ni michuano ya kutafuta kina Onyango wengine na hapana shaka wanafanikiwa kwa mtindo huu. Hadithi hiyo inakwenda kwa Wakenya. Katika michuano kama hii hawawezi kuwaita kina Robert Mambo, Dennis Oliech wala McDonald Mariga wa Parma ya Italia. Hawawezi pia kumuita Mussa Otieno anayecheza Afrika Kusini. Kifupi wenzetu wanaigeuza michuano hii kama vile ambavyo wenzetu wa nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika walivyoigeuza michuano ya COSAFA katika kusaka vipaji vipya. Kule huwezi kuziona sura za akina Collins Mbesuma, Ben McCarthy, Aaron Mokoena, Nasief Morris, Macbeth Sibaya, Sibusiso Zuma, Steve Pienaar, Benedict vilakazi na wengineo wakichezea Afrika Kusini na Zambia katika michuano ya COSAFA. Lakini kwetu michuano ya Chalenji ni fainali kubwa sana. Sielewi ni kwa nini hali hii inatokea kwa wenzetu lakini kwetu ni tofauti. Inawezekana ni kwa sababu hatuna nyota wengi wa kulipwa nje ya nchi na ndio maana tunaigeuza michuano hii kama ëdilií kubwa katika kuwaona nyota wetu. Nakumbuka mwaka jana wakati michuano hii ilipofanyika Ethiopia, kocha Marcio Maximo alijaribu kutumia falsafa ya wenzetu katika kuhakikisha nyota chipukizi wanakwenda na wale wakongwe kina Nsajigwa Shadrack, Victor Costa, Ivo Mapunda na wengineo wanabakia nyumbani. Mashabiki walichachamaa sana bila ya kuelewa falsafa hii rahisi lakini nadhani sasa ni wakati wa kubadili mtazamo na kuangalia ni namna gani tunaweza kuitumia michuano hii. Nafahamu itakapoanza mashabiki na viongozi wa soka watataka mambo makubwa sana kutoka kwa wachezaji na jopo la ufundi, bila kujua namna tunavyoweza kuyatumia mashindano haya katika kukuza zaidi vipaji kuliko kuwatumia sana kina Nsajigwa ambao wameshathibitisha kile wanachoweza kukifanya katika ngazi za kimataifa. Binafsi sijaona hata umuhimu wa kuwaita Danny Mrwanda na Nizar Khafani katika michuano kama hii. Kama wanapata uzoefu wa kweli katika soka la kulipwa ni kiasi cha kuwanyanyua wachezaji wengine tu ili waweze kufikia kiwango chao. Sidhani kama itakuwa vigumu kwa kocha Maximo kuwaunganisha nyota hawa wa kulipwa na wengineo waliopo nyumbani kwa sababu inaaminika nyota wa kulipwa wanafundishwa na walimu wa kisasa wa kiwango cha Maximo huku uwezo wao wa kuelewa ukiwa juu zaidi. Kama mna timu ambayo kwa kiasi chake imeanza kujaribu kucheza na Senegal, Burkina Fasso na Msumbiji, nadhani mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya timu hizi zinaweza kuwa muhimu zaidi kuliko michuano ya Chalenji. Wachezaji wetu wametuangusha kwa kiasi kikubwa. Kama kina Haruna Moshi wangekwenda kucheza soka la kulipwa nadhani ilikuwa nafasi kwetu kuwaona nyota waliochipukia katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoendelea. Lakini kwa akina Haruna kucheza na wachezaji wapya waliochaguliwa na Maximo ni kuyumbisha maana nzima ya michuano ya Chalenji ambayo kwetu tunapaswa kuitumia katika kuanzisha kizazi kingine cha soka kama wenzetu. Kwa barani Ulaya unaweza kuipima michuano hii na ile ya Olimpiki. Timu zinachagua nyota chipukizi na kuongeza nguvu kwa kuchukua nyota watatu wazoefu kwa ajili ya kunogesha timu. Nafikiri kuna tatizo moja litamsumbua sana Maximo. Tatizo la kujua namna ya kukabili michuano inayomkabili pamoja na kukuza soka letu kwa ujumla. Kama kocha amechagua kikosi hiki kwa madai ya kujiandaa na mechi za kufuzu kwenda Kombe la Dunia 2010 pamoja na kuibua vipaji, nadhani kuna kimoja kinaweza kufaulu na kingine kikafeli vibaya. Ni namna gani mashabiki wanaweza kumuelewa, nadhani huo ni mtihani mkubwa kwake kutegemea tu na aina ya mashabiki wetu tulionao nchini. Mwisho wa yote nafikiri itanifurahisha kuona wachezaji wengi waliochaguliwa kwa mara ya kwanza kutoka timu za mikoani wakicheza katika michuano ya Chalenji na kisha wakiibuka kwa kujiamini zaidi, kuliko kuwatumia kina Haruna na kushinda huku tukijifurahisha tu katika nafsi zetu bila ya kusonga mbele. Ni wakati wa kuifikiria upya michuano hii. Wenzetu wanaitumia kwa akili zaidi pengine kuliko sisi ambao unazi umetujaa tukitamani kushinda kila kitu bila ya kujua kama tunasonga mbele au tunarudi nyuma. Naomba kutoa hoja waheshimiwa.